Saturday, July 6, 2019
FAIDA ZA MCHUZI WA PWEZA
Ni maajabu! Pengine hiyo ndiyo sentensi ya haraka itakayotoka kinywani mwako pindi ukisikia namna minofu na supu ya samaki aina ya pweza vilivyo na umuhimu kwa wanandoa.
Kumekuwa na uvumi mwingi mitaani kuhusiana na samaki pweza, ambaye daima hupatikana baharini na kwingineko kujulikana pia kwa jina la utani la ‘paka bahari’. Wengine huwanasibisha pweza na masuala ya kishirikina kutokana na muonekano wake wa kiwiliwili kidogo na rundo la mikia.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa zaidi ya wiki kupitia mahojiano maalumu na madaktari kutoka taasisi kadhaa zikiwamo za Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam umethibitisha kuwapo kwa faida takribani tisa za supu ya pweza mwilini mwa mwanadamu, hususan kwa wale walio katika ndoa na kina mama wanyonyeshao.
Katika uchunguzi wake huo ambao pia ulihusisha mahojiano na baadhi ya wauzaji na walaji wazuri wa pweza, Nipashe imebaini kuwa samaki huyo amejawa na virutubisho vingi vinavyosaidia kuukinga mwili wa mlaji dhidi ya magonjwa kama kansa.
Aidha, pweza amejawa na virutubisho vinavyosaidia kuongeza ashki na kuboresha tendo la ndoa huku pia minofu ya samaki huyo ikiwa na virutubisho vya kumuwezesha mwanamke kuwa na sifa halisi za ‘ukike’ na pia mwanaume kuwa mwanaume wa shoka.
“Mimi sikuwa mlaji wa pweza hadi pale niliposhauriwa kufanya hivyo ili kuiimarisha ndoa yangu. Na kweli, mlo huu (supu ya pweza) umenisaidia sana kwa sababu najihisi kuwa kama kijana. Furaha yangu katika ndoa imerudi,” alisema mkazi mmoja wa Buguruni jijini Dar es Salaam.
VIRUTUBISHO VYA PWEZA
Kwa nyakati tofauti, madaktari waliozungumza na Nipashe walivitaja baadhi ya virutubisho zaidi ya 12 vinavyopatikana kwenye mlo wa supu au minofu ya samaki aina ya pweza ni pamoja na protini, mafuta (fats), vitamini B12, selenium, madini chuma (ron), shaba na pia vitamini B6.
“Virutubisho vyote hivi vinapatikana kwa kiasi kikubwa kwenye minofu ya pweza na karibu vyote ni muhimu katika mwili wa binadamu,” alisema Dk. Damas Mahenda ambaye ni Mhadhiri Msaidizi wa MUHAS.
“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa pweza ana faida nyingi. Na kwa ufupi, unaweza kumuelezea pweza kwa kumlinganisha na kifurushi cha virutubisho muhimu vya mwili wa binadamu. Mnofu wa pweza una protini nyingi kuliko wa kuku.
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa takriban asilimia 10 ya virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini kwa siku hupatikana kwa pweza aliyeivishwa vizuri,” alisema Dk. Mwindah Abdallah wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakati akizungumza na Nipashe juzi.
Akimuelezea zaidi pweza, Dk. Selemani Hassan wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo alisema kuwa samaki wa jamii ya pweza wana faida kubwa mwilini mwa binadamu kwa sababu minofu yao ina virutubisho vya aina nyingi.
“Kuna taarifa nyingi kuhusiana na pweza. Lakini muhimu kuliko yote, na ambayo hutokana na tafiti za kitaalamu, ni kwamba pweza ana manufaa makubwa mwilini. Minofu yake ina virutubisho vingi vinavyohitajiwa mwilini mwa kila mmoja wetu,” alisema Dk. Lugano Mwankemwa ambaye ni Mfamasia katika Hospitali ya Mwananyamala.
Chanzo kingine kinafafanua zaidi kuwa kipande kimoja cha pweza huwa na protini ya kiwango cha juu kwa zaidi ya mara tatu kulinganisha na kipande cha ukubwa sawa cha kuku.
Dk. Emmanuel Mgonja wa hospitali binafsi ya Eden iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam, alisema ulaji wa pweza wenye faida zaidi mwilini unapaswa kuwa walau mara tatu kwa wiki.
“Kwa wiki mlaji wa pweza anatakiwa kula walau mara tatu … lakini ukizidisha siyo mbaya kwa sababu ni chakula cha kawaida,” alisema Dk. Mgonja.
MAAJABU 9
Licha ya pweza kuwa chakula kizuri kinachotumiwa zaidi na watu wa maeneo ya Pwani kama Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara na visiwa vya Zanzibar na Pemba, lakini maajabu yake kuhusiana na namna anavyosaidia kuimarisha afya ya mwili ndiyo huwa gumzo zaidi midomoni mwa wengi.
Katika mahojiano na madaktari waliozungumza na Nipashe, imebainika kuwa virutubisho vya pweza husaidia walau katika maeneo tisa muhimu.
Kwanza, virutubisho vya protini na madini ya selenium ndani ya pweza vinaelezwa kuwa ni baadhi ya vile vinavyosaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa nguvu ya tendo la ndoa wanaume na wanawake.
Dk. Mahenda alisema kuwa baadhi ya virutubishi vya pweza husaidia kuwapa uwezo zaidi wanaume kwa kuongeza idadi ya mbegu zao (sperm count) na pia kuwaongezea ashki ya tendo lenyewe.
“Kwa sababu hiyo, supu ya pweza iliyoandaliwa vizuri inaweza kuwasaidia wanandoa katika kukamilisha jukumu lao la unyumba kwa namna bora zaidi,” alisema Dk. Mahenda.
Aidha, Dk. Mahenda aliongeza kuwa faida ya pili ya pweza ni kuwa na virutubisho vinavyosaidia kuimarisha hali ya ‘uanamke’ na ‘uanamume’ kwa watumiaji.
“Kwa kila mwanadamu huwa kuna vichocheo vya mwili vinavyomtofautisha jinsia yake. Pweza wamejawa na aina ya virutubisho ambavyo husaidia kuimarisha vitabia hivi… kwa mfano, mwanaume kuwa na misuli iliyojengeka zaidi kuliko wanawake na hiyo pia ni faida kwa walaji,” aliongeza Dk. Mwindah wa UDOM.
Jambo la tatu, kati ya virutubisho vya pweza vipo ambavyo husaidia mwili kuukinga dhidi ya maradhi ya kansa. Dk. Mwindah alisema kuwa zipo tafiti zinazoonyesha kuwa watu wanaokula sana pweza huwa na uwezekano mdogo wa kupata kansa mbalimbali zikiwamo za midomo, tumbo, utumbo mkubwa, matiti, shingo ya kizazi, na pia kansa ya mapafu.
“Hili pia ni jambo muhimu kwa wanandoa na watu wengine. Aina ya mafuta ya samaki na hasa ya pweza husaidia kuzalishwa kwa kinga dhidi ya maradhi mengi yakiwamo hayo ya kansa,” alisema Dk. Selemani.
Faida ya nne kwa walaji wa pweza, kwa mujibu wa Dk. Selemani, ni kuwa na virutubisho vinavyosaidia kuukinga mwili dhidi ya kupungukiwa kwa uwezo wa ubongo hasa kwa watu wenye umri mkubwa. Tatizo hilo kitaalamu huitwa Alzheimer.
Tano, pweza huwasaidia walaji kukabili athari za maradhi ya pumu. Dk. Mwankemwa alisema kuwa baadhi ya watafiti wamebaini kuwa mtu anayekula sana pweza huwa na uwezekano mdogo wa kusumbuliwa na ugonjwa wa pumu.
Aidha, alisema kuwa watu ambao tayari wana maradhi ya pumu huweza pia kunufaika na virutubisho vilivyomo kwenye minofu ya pweza kwa kuwapunguzia athari zake, lakini kwa shari kwamba wawe mbali na visababishi vingine vya kuibuka kwa athari hizo.
Faida nyingine ya sita wanayoipata walaji wa pweza ni kuhusiana na kuimarisha uwezo wa mwili katika kufanya kazi mbalimbali zikiwamo za mmeng’enyo wa chakula, upumuaji na hata mzunguko wa damu.
Saba, ni faida ya pweza kwa mwili kuhusiana na maradhi ya kifua na upumuaji. Dk. Selemani alisema kuwa baadhi ya virutubisho vilivyomo kwenye mnofu wa pweza ndivyo huusaidia mwili kufanya kazi hiyo ikiwamo kuimarisha kinga zake dhidi ya maradhi.
“Faida nyingine ni kuongeza uzalishaji wa haemoglobin ambazo ni muhimu katika damu. Hili hufanyika kwa sababu pweza ana madini aina ya shaba ambayo ni muhimu kwa kazi hiyo,” alisema Dk. Selemani wakati akieleza faida ya nane ya matumizi ya pweza.
Dk. aliitaja faida nyingine wanayoipata kina mama wanaokunywa supu ya pweza au kula minofu yake kuwa ni kusaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa pindi wanapojifungua.
Faida nyingine kwa wote (wanawake na wanaume) walao pweza mara kwa mara, kwa mujibu wa Dk. Mgonja, ni kuongeza madini joto mwilini.
Inaelezwa vilevile kuwa vipo virutubisho vya pweza husaidia katika kupunguza athari za baadhi ya maradhi ya moyo kwa sababu ya kuwapo kwa kiwango cha mafuta aina ya ‘omega-3 fatty acids’.
“Kwa ujumla, ulaji wa pweza una faida nyingi mwilini. Kwa wanandoa pia ni muhimu zaidi kwa sababu husaidia kujenga afya ya mwili katika kushiriki vyema tendo la ndoa,” alisema dokta Hassan wa Hospitali ya Kilolo.
ATHARI HASI
Licha ya faida nyingi za supu ya pweza na minofu yake mwilini, Dk. Mgonja na wengine waliozungumza na Nipashe, walitahadharisha juu ya athari hasi zinazoweza kujitokeza kwa walaji wakubwa wa pweza.
Mojawapo ya athari hizo ni kushambuliwa na mzio (aleji) na baadhi ya wale wanaokutwa na athari hizi huwa ni wa kundi la damu la ‘ O’
Hata hivyo, ripoti za tafiti nyingine kuhusiana na ulaji wa pweza zinaonya kuwa samaki huyu hapaswi kutumiwa sana na kina mama wajawazito kwa sababu anaweza kusababisha athari zitokanazo na madini ya zebaki ambayo hupatikana pia mwilini mwake, ijapokuwa huwa ni kwa kiasi kidogo.
WAUZA PWEZA
Katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam, pweza ni maarufu na mara kwa mara huuzwa mitaani nyakati za jioni. Walaji hupata supu inayonakshiwa kwa ndimu na wengine hula minofu ya kuchemsha au kukaangwa.
Baadhi ya wauzaji wazoefu wa samaki huyo waliiambia Nipashe kuwa wateja wapo wa kutosha na kwamba, tofauti na fikra za wengi kuwa walaji wake wengi huwa ni wanaume pekee, ukweli ni kwamba wanawake pia ni walaji wazuri wa supu ya pweza.
“Tofauti ni kwamba kina mama wengi hununua na kwenda kula nyumbani… wanaume hula hapahapa baada ya kununua vipande au kunywa supu,” alisema mmoja wa wauzaji wa pweza nyakati za usiku katika maeneo ya Buguruni.
Mmoja wa wauzaji wa pweza wabichi katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, Hemed Byon, alisema kina mama, hasa wenye umri mkubwa, ndiyo wateja wake wakubwa katika eneo hilo.
“Wanawake wengi huja kununua kwa ajili ya matumizi ya waume zao kwa sababu pweza amekuwa akisaidia kuimarisha ndoa kwa kuwapa nguvu wanaume… pia wanawake ni walaji wazuri wa pweza, hasa wale wanaonyonyesha,” alisema Byon, akiongeza kuwa hivi sasa kilo moja ya pweza huuzwa Sh. 5,500 na wakati mwingine huuzwa hadi Sh. 9,500.
Muuzaji mwingine wa pweza wa kukaanga katika eneo la Feri, Richard Pinde, alisema wateja wake wakubwa ni wanawake.
“Wanawake wanapenda pweza wa kukaanga… baadhi husema wazi kuwa husaidia kuwaongezea nguvu ya kuhudumia ndoa zao,” alisema Pinde huku akicheka
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment